Saturday, October 5, 2013
KATIKA MAPENZI ZINGATIA CHAGUO, SI KILA MFAA MACHO ATAKUFAA -6
BILA kuzingatia chaguo utaendelea kuteswa na mapenzi kila siku. Leo nitamalizia mfano wa Bryson ambao nilianza nao wiki iliyopita. Kwa hakika ukiuelewa, utakupa dira kwenye maisha yako.
Hata hivyo, kabla ya mfano huo, nikumbushe kwamba mapenzi yana nguvu yenye mvutano mithili ya sumaku. Hoja hapa ni kuwa endapo kutakuwa na mapenzi ya kweli, mara nyingi mtajikuta mpo kwenye mstari mmoja. Ni nadra kutofautiana.
Ni lazima itatokea mara chache kutofautiana. Mantiki ni kwamba hata kama mnapendana kiasi gani, haiwezekani kila siku wote mkawa mna mawazo ya aina moja, hivyo mtapingana.
Kuna kukosea, kwa hiyo kibinadamu kuna wakati utamkosea mwenzi wako. Ila uwepo wa penzi la kweli, utasababisha muafaka mapema. Utaguswa kuomba msamaha, naye atahamasika kukusamehe. Mvuto wake ndani yake, utamfanya asichelewe kupitisha msamaha. Hayo ndiyo mapenzi.
Mpenzi wako anayekupenda na kukuamini kupita kiasi, siku ukimtenda ndivyo sivyo, atakaa na maswali mengi kwa muda mrefu. Utageuka kinyaa mbele yake, kwa hiyo hata kukusamehe atapenda kufanya hivyo lakini atachelewa kwa sababu heshima yako kwake, imeondoka kabisa.
Kama inatokea umemkosea jambo dogo lakini anavyolisimamia utadhani umeua mtu. Kama sura ya aina hiyo, inajiri kwenye uhusiano wako, jaribu kutazama mbele kwa matumaini. Huyo hakupendi, atakupotezea muda.
Pengine mapenzi yake kwako ni ya wastani. Ulivyo kwake, ukiwa naye ni sawa na hata usipokuwa naye, ni sawa vilevile. Huyu atakwambia anakupenda muda mwingine kwa sababu anachukulia ni kauli ya mazoea. Ila ukiyatafsiri mapenzi katika kipengele cha mguso wa moyo. Hakupendi, ila amekuzoea.
Kwa mtu wa aina hiyo, mlipaswa kuwa marafiki lakini mkajidanganya mkawa wapenzi. Hizo ni gharama za kulazimisha uhusiano. Elewa kwamba wapo watu ambao ukawa na urafiki nao wa kawaida, halafu yupo mmoja ambaye ndiye mwenye nafasi yake. Anza kufanya upembuzi leo.
Mapenzi si kumuona mtu barabarani akakuvutia basi ukajiaminisha kuwa huyo anakufaa. Mwenzi wa maisha yako ni lazima akidhi vigezo vingi. Wapo ambao utalazimika kuwaacha barabarani wakirandaranda na dunia, halafu yupo mmoja mahsusi anayekufaa kwa hali zote kuwa mwandani wako.
Mfano wa Bryson: Huyu ni msomaji wangu ambaye naomba nimtaje kwa jina hilo. Alinilalamikia kuhusu tabia ya mkewe. Akadai kuwa wakati mwingine hafikirii kama aliyemuoa ni mke wake, ila changudoa anayetaka kuvuna kwake. Akaenda mbali zaidi kwa kusema anahisi mkewe ana kidumu nje ya ndoa yake.
Akaeleza kwamba yeye na mkewe tofauti yao kubwa huwa ni usiku wakati wa kulala.
Itaendelea . . .