Sir Alex Ferguson aamua kustaafu |
Sir Alex Ferguson anastaafu akiwa
amedumu kwa karibu miaka 27 na karibu michezo 1500 aliyoifundisha
Manchester United. Katika taarifa ya United iliyotoka mapema asubuhi ya
leo, imesema Uamuzi huo haukuwa jambo dogo kuafikiwa lakini umekuwa ni
uamuzi kwa wakati sahihi.
Ndiye meneja mwenye mafanikio zaidi
katika historia ya soka la Uingereza ambapo ameshinda mataji 13 ya ligi
kuu, Mataji mawili ya Klabu bingwa barani Ulaya na matano ya kombe la
FA.
Ferguson ambaye ni raia wa Scotland, mwenye umri
wa miaka 71 amehitimisha tetesi ambazo zilikuwa zikivuma tangu jana
kuwa huenda angestaafu mwishoni mwa msimu huu na Mchezaji wa zamani wa
Manchester United Pad Crerand anasema haujui maisha yatakuwaje Old
Traford bila ya Ferguson maarufu kama Fergie.
Uvumi tayari umekwishatanda juu ya nani atakuwa
mrithi wake,ambapo meneja wa Everton Mscotland David Moyes ametajwa
sana, huku wengine wakimtaja Jose Mourinho na pia taarifa zingine
zikimtaja kocha wa Borusia Dortmund Jurgen Kloop japo taarifa hizo
zimekanushwa na Klabu hiyo muda mfupi uliopita.
Ferguson atawaaga rasmi mashabiki wa United
jumapili ijayo wakati timu hiyo ikikabidhiwa kombe katika mchezo dhidi
ya Swansea lakini ataendelea kuwa sehemu ya Manchester United ambapo
sasa atakuwa balozi wa heshima wa United na kuwa mjumbe wa bodi ya
wakurugenzi ya klabu hiyo.