Sina uhakika sana ila naanza kuandika hiki kipande nikiamini kwamba
unajua nini maana ya mitandao ya kijamii(social networks). Siku hizi
makampuni makubwa makubwa duniani yanaajiri wataalamu wa kitu
kinachoitwa New Media/Social Networks.Wengi wao ni vijana wadogo tu
ambao aidha ndio wametoka vyuoni au wamejiari kwa kutumia mitandao
jamii.
Leo naomba nigusie kidogo mtandao wa Twitter
na kwanini nashauri ujiunge nao.Endapo unatumia e-mail hivi leo basi ni
wazi kwamba kama bado hujajiunga au kufungua akaunti yako ya
Twitter,basi hivi karibuni itakubidi. Mimi binafsi ni mtumiaji wa
Twitter japokuwa siwezi kujiita mtumiaji mkubwa kwani bado sijafikia
spidi ya kupost zaidi ya mara kumi kwa siku.Spidi zangu zinatofautiana
Sababu ya Kwanza: Ni vizuri mapema kabisa ukachukua
username yako. Kila siku majina ya watu yanazidi kuchukuliwa.Hakikisha
umechukua lako mapema kwani tofauti na mitandao inayotoa huduma za barua
pepe(e-mail),mtandao wa twitter.com ni mmoja tu. Kwa hiyo ukikuta jina
lako limechukuliwa utakuja kuishia au kupaswa kuchukua jina kama
jumapachu76654256 kwa sababu tu twitter.com/jumapachu itakuwa imechukuliwa
Sababu Ya Pili: Nenda na wakati kwa kuelewa
kinachoendelea katika ulimwengu wa tekinolojia ya mawasiliano.Hili ni
muhimu zaidi kama una watoto au unatarajia kuwa na watoto. Mimi nina
watoto.Ni muhimu kujua kinachoendelea mtandaoni kwani watoto wa siku
hizi,tofauti na enzi zetu,wao ni watumiaji wazuri zaidi wa mitandao.Na
huko,kwa bahati mbaya,wapo watu wasio na utu wala maadili.Usiposimamia
usalama wao,utakuwa unafanya makosa kama mzazi.Chukua hatua,nenda na
wakati.
Sababu Ya Tatu: Ni jambo la hakika kwamba ukianza kutumia Twitter
au mitandao jamii mingine,utajifunza mambo kadhaa na bila shaka
utafurahia. Kama unapenda kusikia “umbea” au udaku utaukuta katika Twitter.Kama
unapenda kujua mambo kadhaa kuhusu maendeleo ya ulimwengu wa
mtandao,habari za papo kwa papo(breaking news),habari za masoko ya
hisa,nk.Yote hayo unaweza kuyapata kwa haraka sana kupitia mtandao wa
Twitter.
Sababu Ya Nne: Kama una wasiwasi au uoga kwamba mtandao wa Twitter
pengine ni mgumu sana kuuzoea au kuutumia,naomba nikuhakikishie kwamba
ni rahisi sana kuutumia.Lugha inayotumika,ujuzi au ufundi wa kuingia na
kutoka,kutuma vitu,nk ni jambo rahisi sana kulielewa.Ukishaanza tu
kuutumia,utaona jinsi wengine wanavyofanya na utaelewa ilivyo rahisi.Kwa
hiyo ni rahisi kuutumia,shaka ondoa.
Sababu Ya Tano: Baadhi ya watu wamewahi kuniambia
kwamba wanahofia kutumia mitandao ya kijamii ikiwemo Twitter kwa kuhofia
usalama wa habari zao au kupunguza uwezo wako wa kufikiri(zimewahi
kutolewa hoja za namna hiyo kwa wanaopinga matumizi ya Twitter na
mitandao jamii mingine).Kama ilivyo rahisi katika kujiunga ni rahisi pia
kujiunga bila kujulikana na kila mtu(labda wewe mwenyewe na watu wako
wa karibu sana) na pia ni rahisi kujitoa.Usalama upo.Habari kwamba
Twitter wanachofanya ni kuisaidia serikali ya Marekani katika kukusanya
taarifa za watu,nchi nk hazina msingi wala utafiti wa hakika wa
kiinteligencia.
Sababu Ya Sita: Twitter na mitandao mingine ya
kijamii sio sehemu tu ya “wateja” au “walevi” wa masuala ya mitandao au
jamii, ni sehemu ya watu wote wanaopenda kujifunza jambo moja au jingine
kutoka kwa watu au kubadilishana maarifa. Kwa mfano,mojawapo ya mambo
ambayo mimi binafsi nayafurahia sana katika utumiaji wangu wa mtandao wa
Twitter ni pamoja na kusoma au kupata habari.Kwa sababu takribani
vyombo vyote vya habari duniani vinazo akaunt zao maalumu za
Twitter,basi upatikanaji wa habari zote muhimu kupitia mtandao huo ni
rahisi. Utasoma na kujifunza mengi kutoka kwa watu,vyombo vya habari
nk.Jiunge na Twitter leo. Bonyeza hapa kufanya hivyo.
Je,kama wewe unayesoma habari hii tayari unatumia mtandao wa
Twitter,nini maoni yako kuhusu Twitter.Unakubaliana na sababu hizo hapo
juu? Unazo za nyongeza au za kupunguza? Account yako ya Twitter ni ipi ili “tukufuate”?