Tatizo
la kukosa hedhi ni jambo ambalo linawakumba wanawake wengi waliovunja
ungo. Aidha suala hili limekuwa likiwaletea usumbufu mwingi wa
kisaikolojia wanawake wengi waliowahi kukumbana nalo.Tatizo la kukosa
hedhi au amenorrhea linaweza kutokea awali kabisa (primary) au baadaye
kabisa maishani (secondary).
Primary amenorrhea ni hali ya kukosa
hedhi inayoweza kumtokea msichana aliye katika umri wa kuvunja ungo na
ambayo huweza kuendana na hali ya kukosa mabadiliko ya kubalehe kama
vile kuota matiti au nywele za kinena; au msichana anaweza kuwa na
mabadiliko ya kubalehe lakini asipate hedhi.
Secondary amenorrhea
ni hali ya kukosa hedhi inayomtokea mwanamke ambaye si mjamzito,
hanyonyeshi, na ambaye hajavuka umri wa kukosa hedhi (menopause) na wala
hatumii njia za uzazi wa mpango kama vile sindano au vidonge, na ambaye
hapo awali alikuwa akipata hedhi kama kawaida lakini akasimama kwa
miezi mitatu au zaidi.
Mwanamke hupataje hedhi?
Ili mwanamke
aweze kuwa na mzunguko ulio sahihi wa hedhi, ni lazima matezi yake ya
hypothalamus napituitary pamoja na kiwanda cha kutengeneza mayai ya kike
(ovaries) na mji wa mimba (uterus) vifanye kazi zake sawasawa.
Amenorrhea husababishwa na nini?
Visababishi
vya amenorrhea vyaweza kugawanywa katika makundi makuu matatu, vile
vinavyohusisha matatizo katika mfumo wa homoni, vile vinavyohusisha
matatizo ya kimaumbile katika njia ya uzazi ya mwanamke na vile
vinavyohusisha mabadiliko katika mwili wa mwanamke.
1. Matatizo
katika mfumo wa homoni: Matatizo katika mfumo wa homoni yanaweza kuwa
katika tezi za hypothalamus, pituitary au ovary.
1. Matatizo katika Hypothalamus: Matatizo katika hypothalamus yanayoweza kusababisha mwanamke kukosa hedhi ni pamoja na
-Uvimbe katika ubongo karibu na tezi ya pituitary
-Ukosefu
au upungufu wa homoni zinazochochea kukua na kufanya kazi kwa via vya
uzazi. Ugonjwa huu hujulikana kama Kallmann syndrome
-Lishe duni na utapia mlo
-Uzito mdogo kuliko kawaida (kukonda kwa kupitiliza)
2. Matatizo katika tezi ya Pituitary: Vyanzo vinavyohusisha tezi ya pituitary ni pamoja na
-
Kuwepo kwa kiwango kikubwa cha homoni ya prolactin katika damu au kwa
kitaalamuProlactinemia. Prolactin ni homoni inayochochea uzalishaji wa
maziwa wakati wa kunyonyesha. Hali ya kuwa na prolactin nyingi katika
damu inaweza kutokea iwapo kuna uvimbe unaoitwa (prolactinoma) katika
tezi ya pituitary.
-Kuwepo kwa uvimbe mwingine wowote katika tezi ya pituitary.
-Pituitary kushindwa kufanya kazi baada ya seli zake kufa, hususani iwapo mama alipoteza damu nyingi wakati wa kujifungua.
-Kuharibika kwa tezi ya pituitary baada ya seli zake kushambuliwa na mfumo wa kinga ya mwili.
-Kuwa na historia ya kupata tiba ya mionzi inayohusisha tezi ya pituitary.
3. Matatizo katika ovary: Vyanzo vinavyohusisha matatizo katika viwanda vya kuzalisha mayai ya kike yaani ovaries ni pamoja na
-Kutozalishwa kabisa kwa mayai (Anovulation)
-Kuwepo kwa kiwango kingi cha homoni za kiume katika damu (Hyperandrogenemia)
-Ovary
kuwa na vifukovifuko (Polycystic ovarian syndrome) na kushindwa kufanya
kazi zake vizuri. Haya ni matatizo ya homoni ambayo huwapata baadhi ya
wanawake walio katika umri wa kuzaa
-Kufa na kushindwa kufanya kazi kwa ovary kabla ya muda wake
-Ugonjwa
wa kuzaliwa unaoitwa Turner syndrome ambao humbatana na kukosekana kwa
ovary au ovary kuwa changa kuliko kawaida, msichana kushindwa kuvunja
ungo na msichana kuwa na kimo kifupi kuliko kawaida. Ugonjwa huu
hutokana na matatizo ya kijenitikia (genetic disease)
-Ukosefu wa kimaumbile wa ovary ambao hutokea wakati wa ukuaji
-Kufa kwa ovary baada ya seli zake kushambuliwa na mfumo wa kinga ya mwili
-Historia ya kuwahi kupata tiba ya mionzi au madawa yanaathiri ovary
-Ugonjwa wa kurithi wa Galactosemia unaoambatana na kuwa na kiwango cha juu cha sukari aina ya galactose katika damu
2.
Matatizo ya kimaumbile katika njia ya uzazi: Matatizo ya kimaumbile
katika njia ya mfumo wa uzazi wa mwanamke yanayoweza kusababisha ukosefu
wa hedhi ni pamoja na
1. Mwanamke/msichana kuzaliwa bila kuwa na uke, shingo ya uzazi au mji wa mimba (uterus)
2. Kuta za uterus zinazotazamana kujishikiza pamoja
3. Utando unaozunguka uke (hymen) kuziba kabisa na kukosekana kwa tundu la kupitishia damu ya hedhi (imperforate hymen)
4. Kuwepo kwa utando unaokatiza katika uke unaozuia damu ya hedhi kushindwa kutoka
3.
Mabadiliko katika mwili wa mwanamke: Mambo yanayoweza kuathiri mwili wa
mwanamke na kumfanya ashindwe kupata hedhi ni pamoja na
1. Kula kiasi kidogo sana cha chakula kuliko kawaida au kula kupita kiasi
2. Unene uliopitiliza au kupungua uzito/kukonda isivyo kawaida
3. Uwepo wa magonjwa sugu kama kifua kikuu
4. Utapiamlo
5. Msongo wa mawazo
6. Matumizi ya madawa ya kulevya
7. Matumizi ya baadhi ya madawa hususani baadhi ya dawa za kutibu magonjwa ya akili
8. Kuwa na hofu iliyopitiliza
9. Kufanya mazoezi ya mwili kupita kiasi
Dalili za Amenorrhea ni zipi?
Kukosa
hedhi siyo ugonjwa bali ni dalili ya kuwepo kwa tatizo au ugonjwa
fulani katika mwili. Kulingana na ugonjwa unaosababisha tatizo hili,
kukosa hedhi kunaweza kuambatana pia na
• Matiti kutoa maziwa wakati
mwanamke si mjamzito na wala hanyonyeshi, maumivu ya kichwa na matatizo
katika kuona vitu ambavyo kwa pamoja vinaweza kuashiria uwepo wa uvimbe
katika ubongo
• Mwanamke kuwa na nywele na vinyweleo vingi mwilini na
kuota ndevu kama mwanaume hali inayoashiria kuwepo kwa wingi kwa homoni
za kiume za androgen
• Ukavu katika uke, kutoka jasho sana wakati wa
usiku, au mabadiliko katika kupata usingizi vinaweza kuashiria matatizo
katika ovary
• Kuongezeka uzito kupita kiasi au kupungua kwa uzito isivyo kawaida
• Mwanamke kuwa na mhemko kuliko kawaida yaweza kuashiria kuwepo kwa matatizo ya kiakili na kisaikolojia
Je kukosa hedhi kunaweza kusababisha nisipate mtoto?
Ikumbukwe
kuwa, kukosa hedhi si ugonjwa bali ni dalili ya kuwepo tatizo hivyo
basi iwapo tatizo hilo lina uhusiano na kutunga mimba na kupata mtoto,
uwezekano wa kupata mtoto utakuwa mdogo ikiwa tatizo hilo
halitashughulikiwa.