Headlines News :

Saturday, March 9, 2013

LETTER TO FACEBOOKERS


BARUA KWA WANAFACEBOOK
Kwako Kaka,

Usione nimekaa kimya sana huku uswahilini ukaanza kusema kwamba nimekutenga, hapana, bado nakukumbuka sana kaka yangu mpendwa. Toka ulipotuhama na kuhamia Masaki, nimekuwa mtu mnyonge sana, nashinda peke yangu huku simu uliyoniachia ikiwa mkononi mwangu.
Leo kaka ningependa kukuambia kitu kimoja, hasa mtandao huu wa Facebook ambao ulikuwa ukiniambia sana nisijiunge nao kwani nisingeweza kusoma. Niliyapuuzia sana maneno yako ila kwa sasa ndio naona madhara ya mtandao huu.

Leo nitakwenda kukuambia machache juu ya mtandao huu wa facebook ambao unatumiwa na simu zote

zenye uwezo wa kuunganisha internet kama hii yangu, siwezi kuongelea kuhusu BBM kwa sababu sina Blackberry na wala siwezi kuongelea Watsup kwa sababu sina simu ya Nokia, kwa sababu natumia Tecno kuingia facebook, acha niuzungumzie mtandao huu wa facebook.
Unakumbuka kwamba nilipokuwa kidato cha pili nilikuwa kichwa darasa zima, nakumbuka nilikuwa napata hesabu 90%, Book-keeping 98% na masomo mengine kwa alama za juu sana ila kwa sasa nimeshuka kwa kiwango kikubwa sana, sijui itakuwaje nitakapofanya mtihani wa Taifa mwakani.
Kaka jinsi nilivyofikiri kumbe si ukweli ulivyo. Kipindi cha mwanzo nilifikiria kwamba Facebook ni sehemu ya watu kuwa marafiki tu kumbe kuna mambo mengi sana ambayo hutokea nyuma ya pazia. Juzi juzi nilikuwa nimepata habari kwamba kuna msichana wa Kinaigeria kauawa, kisa facebook huku hata wengine wakiamua kutembea nje ya ndoa zao.
Unamkumbuka yule msichana wangu? Sasa hivi nimemuacha bwana eti kisa nimekutana na msichana mzuri huku Facebook, dah! Yaani sijui niseme nini kaka. Facebook imekuwa sehemu ya matatizo makubwa sana katika maisha yangu, muda wote naiwaza hiyo tu.

Kasi yangu ya kwenda kanisani imepungua kabisa na hata kama nitakwenda basi itakuwa ni lazima niwe nachati Facebook kisiri siri huku nikiweka post ya baadhi ya mambo ambayo yanaonekana kanisani, kaka, niombee, hali si shwari kabisa.
Mpaka sasa hivi kaka ukiniuliza facebook imenipa faida gani, sina cha kujibu ila ukiniuliza hasara, zipo nyingi sana. Imenifanya hata kutokwenda kumsalimia dada, salio ambalo mara nyingi huwa unanitumia la shilingi 500 ili niwe nawasiliana na mama na kumjulia hali, mimi najiunga na huduma ya internet na kisha kuingia facebook.


Siku hizi usiku nimekuwa popo, nachelewa sana kulala na ninawahi sana kuamka. Tetesi za watu kufa, zote huwa ninazitolea humu, skendo za mastaa wengi huwa ninazitolea humu. Unakumbuka kipindi kile ambacho nilikwambia kwamba kama ningejiunga na Facebook marafiki zangu wangekuwa wazungu tu ili nipate bahati kama aliyoipata Baraka Kyomo ya kupendwa na mzungu wa Marekani na sasa hivi anakula bata? Mpaka leo mwaka wa tatu sasa, sijampata mzungu yeyote.
Kuna matukio mengi sana huwa yanatokea humu kaka. Kuna mwanamke mmoja anaitwa Suzan, huyu alikutana na mwanaume facebook, akazoeana nae sana na mwisho wa siku wakawa wapenzi. Mapenzi yaliendelea lakini Suzan hakuwahi kuiona sura ya mpenzi wake anayechati nae, akalilia sana kuiona picha ya mpenzi wake.

Mwanaume huyo akamwambia sawa, ila usishtuke mara utakapoiona picha yangu nitakayoiweka, Suzan akajibu sawa. Kaka huwezi kuamini, ndio maana nakwambia kwamba mtandao huu siku hizi hata mashetani nao wanautumia sana, baada ya mwanaume huyo kuiweka picha yake kwenye mtandao huu, Suzan alipoiona tu, akaingiwa na mapepo ambayo baadae yakapelekea kuwa chizi na kugongwa na gari pale Magomeni Hospitali na kufariki papo hapo!.
Ukiachana na huyo Suzan kaka, kuna mwanaume mwingine anaitwa Pawasa ambaye alimpata rafiki wa kiume kutoka nchini Australia, wakawa marafiki sana, mwisho wa siku mwanaume yule akamtaka Pawasa aelekee Australia. Pawasa alifurahi sana, na kweli alipokwenda huko, akakutana na rafiki yake huyo ambaye alimtumia tiketi na kumpa barua ya mwaliko.
Kaka….kaka…kaka amini usiamini, baada ya kufika katika nyumba ya mwanaume huyo, Pawasa akapewa kinywaji kilichotiwa dawa, alipokunywa tu, akalewa na baada ya hapo kuingiliwa kimaumbile na huyo jamaa. Mungu wangu! Kwa sasa ninavyoongea, Pawasa kawa shoga mkubwa sana ambaye anajulikana sana nchini Australia.

Facebook imeniogopesha kaka, hasa hasa kwa hawa watu ambao hawataki kuweka picha zao na kila siku wanataka nichati nao. Huwa ninajiuliza sababu ambazo zinawafanya kutokuweka picha zao ni zipi lakini sipati jibu kabisa.
Maisha ya huku facebook yapo tofauti sana, kuna watu wanapenda sana sifa, utawakuta wengine wanasema wapo Samaki Samaki wanapata lunch na wakati wakati huo huo nipo nao huku Tandale. Na wengine wanadiriki kuandika wanasoma UDSM na wakati ni mabeki 3 (wafanyakazi wa ndani) hapo Magomeni.

Ukiachana na hao wapenda sifa kaka, kuna wengine yaani wao wanajidai kuwa watawala, yaani utafikiri mtandao wa facebook ni mali yao kaka. Wewe unaweka picha halafu mtu anakuja na kukuambia itoe hiyo picha eti kisa hajaipenda, utafikiri nimemuwekea yeye, yaani maisha yao yamekuwa yakiwaambia kwamba wanatakiwa kuwa watawala kila kona.
Kaka…..kaka..kaka hivi unajua kwamba siku hizi hata biashara fulani fulani zimehamia facebook? Rafiki yangu Jumanne siku hizi wala ahangaiki kama zamani, akitaka tu, anamu-inbox, wale wa kule kwa Macheni, Kinondoni wanakuja, yaani ni hatari sana kaka.
Kusema ukweli pamoja na mambo hayo yote lakini kwa asilimia chache facebook imeweza kunielimisha sana, imenifundisha kwamba ni watu wa aina gani ambao natakiwa kuwa nao. Wengine hawafai kaka, yaani wao kila siku wanaweka post kuhusiana na mapenzi, asubuhi mapenzi, mchana mapenzi na usiku mapenzi, kama watu hawa wakiwa marafiki zangu unafikiri na mimi nitakuwa mtu wa aina gani kaka, hauoni kama nitaweza kuwapenda mpaka binamu zangu na kuanzisha kizaazaa kwa mjomba?
Kaka, kama una lengo la kufungua akaunti facebook, achana nayo kabisa, ukija huku unaweza ukamuacha mke wako ndani ya mwezi mmoja tu, ukija huku unaweza ukawa unachelewa kulala kaka, ukija huku pia unaweza ukawa unapata makwazo kila siku, watu wengine wanakera sana.

Nitakuandikia mengi ambayo yanajili huku, ila hayo ni machache sana, siku nyingine, nitakuandikia tena. Utakapomaliza kuisoma hii barua naomba uichane kwani shemeji akiiona anaweza akamwambia mama kwamba nina akaunti facebook, si unajua mama akijua inakuwaje, ataweza kunipokonya hata hii simu ya mchina ambayo umenipa.
Naomba uwasalimie wote huko Masaki. Nimeamua kukuandikia barua na si kukupigia simu kwa sababu simu yangu haikuwa na salio la kutosha, 500 ambayo ulinitumia jana nilijiunga na internet ili niingie facebook. Nimeamua kukuandikia hii barua kwa sababu jana baba alisema kwamba leo angekuja kukutembelea, na ndio maana nimeandika na kumpa.

Siku njema kaka. Nitakuja huko pamoja na huyu msichana wangu wa facebook ili tuje tukusalimia kaka. Nakutakiwa siku njema. Mpe Hai Shemeji pamoja na mtoto wako, Junior.

[Umeipenda? bonyeza kwenye "SHARE" ili na marafiki zako waone na wasome kupitia  Twitter /Facebook 


      JUST COMMENT YOUR OPINION!
  •  
    Support : Blog designer | Blogger | Developer | | KakyteeMedia.InC
    Copyright © 2011. Kakytee.com - All Rights Reserved
    Template Modified by KakyteeMedia
    Proudly powered by Blogger