"Daktari nisaidie, nakufa mie" Wagonjwa wengi husema
wanapoingia chumba cha daktari, wakiongea kwa taabu sana, huku wakipumua kwa
taabu na mlio kama wa filimbi ukisikika. Madaktari huuliza maswali machache na
kugundua ni PUMU.
PUMU ni ugonjwa sugu ambao huathiri njia ya hewa ambazo
huingia na kutoa hewa katika mapafu. Upatapo ugonjwa wa pumu, kuta za ndani za
njia ya hewa huvimba na hivyo kupunguza kiasi cha hewa kinachoingia na kutoka
kwenye mapafu. Hali hii husababisha muathirika kutoa mlio kama wa filimbi au
mluzi wakati wa kupumua, kifua kubana, kushindwa kupumua vizuri na kukohoa.
Watu wenye pumu hupatwa na dalili hizi mara nyingi nyakati za usiku na asubuhi
sana.
Kulingana na takwimu za hivi karibuni, huathiri watu
milioni 300 duniani kote na zaidi ya milioni 22 wakiwa Marekani peke yake.
Ingawa ugonjwa huu huathiri watu wa rika zote, lakini mara
nyingi huanza utotoni, huathiri watoto milioni 6 nchini Marekani. Ugonjwa wa
pumu huua watu 255,000 duniani kote kila mwaka.
AINA ZA PUMU
PUMU YA UTOTONI (Child-Onset Asthma)
Hii ni aina ya pumu inayotokea baada ya mtoto kuwa kwenye
vizio kama vumbi la wadudu mfano mende, manyoya ya wanyama wa kufugwa kama paka
na mbwa. Pumu hii hutokea kwa kuwa mwili wa mtoto hutengeneza kingamwili
(Antibodies) za IgE zinazosababisha pumu.
Ugonjwa wa pumu ni ugonjwa sugu uliopo sana kwa watoto
waliozaliwa na uzito mdogo, wenye asili ya kiafrika, walio katika mazingira ya
moshi pia waliolelewa latika mazingira ya dhiki/umaskini.
Watoto wengi huanza kuonyesha dalili wakikaribia miaka
mitano. Huanza kama ugonjwa wa njia ya hewa kama mafua na kikohozi.
Watoto wa kiume wana hatari zaidi ya kupata pumu
ikilinganishwa na watoto wa kike, ila hali hii huwa kinyume kipindi cha utu
uzima.
Watafiti wanafikiri hali hizi huwapata watoto wa kiume
zaidi kwa kuwa na njia za hewa nyembamba zaidi ikilinganishwa na njia za hewa
za watoto wa kike. Hali hii hupelekea watoto wa kiume kuwa kwenye hatari zaidi
wanapopatwa na maambukizi ya virusi mfano mafua.
PUMU YA UKUBWANI (Adult-Onset Asthma)
Pumu hii huanza baada ya kufika miaka 20. Pumu hii huathiri
sana wanawake kuliko wanaume na pia haitokei sana kama pumu ya utotoni. Vizio
pia husababisha aina hii ya pumu.
Inakadiriwa kuwa 50% ya pumu ya ukubwani husababishwa na
vizio na aina hii ya pumu huitwa pumu ya ukubwani ya vizio ( Allergic
adult-onset asthma). Na 50% haisababishwi na vizio (Allergens) nayo hujulikana
kama pumu ya ukubwani isiyosababishwa na vizio (Non-allergic adult-onset
asthma/Intrinsic asthma).
PUMU ITOKANAYO NA MAZOEZI (Exercise-induced asthma)
Ikiwa utakohoa na kukosa pumzi wakati wa mazoezi au baada
ya mazoezi, inawezekana una pumu inayosababishwa na mazoezi. Ingawa kama sio
mtu wa michezo kukimbia kwa kasi kwa angalau dakika 10 kunaweza kusanabisha
kukosa pumzi na kukohoa. Ikiwa utakohoa na kukosa pumzi kwa muda mrefu basi hii
itaonyesha una pumu inayosababishwa na michezo.
PUMU ITOKANAYO NA KUKOHOA (Cough-Induced Asthma)
Ni aina ngumu ya pumu kwa daktari kuweza kuigundua. Kwenye
pumu hii inawezekana zisitokee dalili zingine zaidi ya kukohoa. Madaktari
hulazimika kuchunguza sababu zingine za kukohoa sana na kuhakikisha sio
zinazosababisha kukohoa huko.
PUMU ITOKANAYO NA KAZI (Occupational Asthma)
Aina hii ya pumu humtokea mtu akiwa mahali pake pa kazi.
Huwatokea sana watumishi wa viwandani ambapo kuna kemikali, moshi na gesi
(Nitrogen oxide) zinazoweza kuamsha pumu.
PUMU YA USIKU (Nocturnal Asthma)
Pumu hii hutokea kati ya saa 6 usiku na saa 2 asubuhi. Pumu
hii huamshwa na vumbi, halufu kali kama za rangi ya nyumba na halufu ya vinyesi
vya wanyama wa kufugwa. Mara nyingi wagonjwa hushtuka usingizini wakati wa
usiku wa maanani baada ya kukosa pumzi.
PUMU KALI/PUMU ISIYOKUBALI STEROIDI (Severe
Asthma/Steroidal-Resistant Asthma)
Wakati wagonjwa wengi wa pumu hupata nafuu baada ya
matumizi ya steroidi, wachache hawapati nafuu. Hivyo wagonjwa hawa huhitaji
matababu bora zaidi ya matibabu ya kawaida.
NINI HUSABABISHA PUMU?
Visababishi vya pumu havijulikani waziwazi, ingawa vitu
vinavyoongeza hatari ya kupata pumu ni vizio mfano moshi, harufu, gesi na
kemikali.
Kila mgonjwa wa pumu ana mzio. Zaidi ya 25% ya watu hupatwa
na mafua yasababishwayo na mzio (Hay fever/Allergic rhinitis) na kuwashwa macho
(Allergic conjuctivitis) pia wanaweza kupata pumu.
Mzio unaweza sababishwa na kingamwili (Antibodies) zilizo
ndani ya damu zinazopelekea njia ya hewa kuvimba na kusababisha pumu.
Vizio vinasababisha sana pumu ni kama moshi, vumbi kutoka
kwenye manyoya ya wanyama kama paka na mbwa, wadudu kama mende na halufu kali
kama za manukato.
Moshi wa sigara unahusishwa sana na hatari ya kupata pumu
pia hatari zaidi ya kufa kwa pumu. Watoto wa wazazi wanaovuta sigara wapo
katika hatari ya kupata pumu. Pia watu wazima wanaovuta sigara wapo katika
hatari ya kupata pumu.
Sababu zingine za kimazingira kama halufu (Marashi)
inayosababishwa na vitu vya kusafishia nyumba pamoja na rangi za nyumba, hewa
itokanayo na majiko ya gesi (Nitrogen oxide).
Uchafuzi wa mazingira kutokana na gesi (Sulfur dioxide,
Nitrogen oxide) pia mazingira ya baridi huamsha ugonjwa wa pumu. Vitu hivi
husababisha njia za hewa kusinyaa na kusababisha matatizo ya kupumua.
Watu wazima wenye uzito unaozidi kimo chao yaani wenye Body
Mass Index (BMI) kati ya 25 na 30 wanaweza kupata pumu kwa 38% ikilinganishwa
na watu wazima wenye uzito wa kawaida. Watu wanene zaidi wenye BMI ya 30 au
zaidi wapo katika hatari mara mbili.
Watoto waliozaliwa kwa njia ya upasuaji wana hatari ya kupata
pumu kwa 20% ikilinganishwa na watoto waliozaliwa kwa njia ya kawaida. Pia
wajawazito wanaovuta sigara hupunguza utendaji wa mfumo wa hewa wa mtoto aliye
tumboni hivyo huongeza hatari ya mtoto kupata pumu. Utafiti umeonyesha pia
mtoto aliyezaliwa na uzito mdogo yupo kwenye hatari ya kupata pumu pia.
Watu walio na msongo wa mawazo (Stress) wapo katika hatari
kubwa ya kupata pumu kwa kuwa watu wengi wenye msongo wa mawazo hujaribu
kujituliza kwa kutumia vileo na kuvuta tumbaku hivyo kuongeza uwezekano wa
kupata pumu. Ingawa utafiti wa hivi karibuni umegundua mfumo wa kingamwili
hubadirika kutokana na msongo wa mawazo (Stress) kitu kinachoweza kusababisha
kutengenezwa kwa kingamwili (Antibodies) za igE zinazosababisha pumu.
Chembe za urithi pia huhusianishwa na ugonjwa wa pumu. Kuna
chembe za urithi 100 zinazohusianishwa na pumu. Uwezekano wa kupata pumu
kutokana na lurithi kwa wazazi ni 3 ya 5. Taasisi za kudhibiti magonjwa ya
Marekani (The Centers for Disease Control USA) zinasema kuwa na wazazi wenye pumu
huongeza hatari ya mtoto kupata pumu pia mara 3 hadi 6.
Tatizo la ngozi linalosababishwa na mzio/allergy
(Eczema/Atopic dermatitis). Watoto 40% hadi 50% wenye tatizo hili hupatwa na
pumu na inawezekana wenye tatizo hili hubanwa na pumu ya mara kwa mara.
DALILI ZA PUMU
Sio watu wote wenye pumu huwa na dalili hizi. Vilevile kuwa
na dalili hizi hakumaanishi una ugonjwa wa pumu.
=> Kukohoa. Kikohozi kinachotokana na pumu huwa kinakuwa
kikali sana hasa wakati wa usoku au asubuhi sana.
=> Kutoa sauti kama filimbi au mluzi wakati wa kupumua.
=> Kubanwa kifua. Mgonjwa huhisi kama kifua kinabanwa na
kitu au kuna kitu kizito kimewekwa juu ya kifua.
=>Kupungukiwa na pumzi. Wagonjwa wenye pumu huhisi pumzi
imekosekana, zaidi inakuwa ni ngumu kutoa pumzi kutoka katika mapafu.=
JINSI YA KUTIBU & KUDHIBITI PUMU
Pumu ni ugonjwa sugu usiotibika ila unaweza kudhinitiwa.
Ili kudhibiti ugonjwa huu, uhusiano mzuri kati ya mgonjwa na daktari
unahitajika sana.
Ili kudhibiti yafuatayo huhusishwa :-
=> Kuzuia dalili hatari kama kukohoa na kupungukiwa na
pumzi.
=> Kupunguza uhitaji wa dawa za kutuliza maumivu haraka
kama Aspirin
=> Kufanya kazi kwa kiasi na kulala vizuri wakati wa
usiku.
- See more at:
http://www.fikrapevu.com/mambo-muhimu-ya-kufahamu-juu-ya-pumu-asthma-na-matibabu-yake/#sthash.LMU827X6.dpuf