HATIMAYE kocha, Jose Mourinho, amekubali kuinoa tena Chelsea kwa mkataba mnono wa pauni 10 milioni na kumekuwa na taarifa kwamba atatua rasmi Stamford Bridge, Julai Mosi. Habari zinasema kocha huyo wa Real Madrid alikutana na mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich na kupata chakula cha usiku kwenye mgahawa wa La Famiglia jijini London ambapo walifanya mazungumzo ya kina na kocha huyo alikubali kutua Chelsea kwa dau hilo. Hata hivyo kocha huyo atatakiwa kuweka mambo sawa kati yake na uongozi wa Real Madrid kwa kuwa bado ana mkataba kwenye klabu hiyo unaomalizika baada ya miaka mitatu. Habari zinasema Abramovich atatakiwa kutoa kiasi cha pauni 12 milioni kwa Real Madrid ikiwa ni gharama ya kuvunja makataba wa kocha huyo. Chelsea itamtambulisha kocha huyo kabla ya kuanza kwa ziara za mechi za kirafiki, hiyo inamaanisha kuwa mechi ya kwanza ya kocha huyo itakuwa dhidi ya Singha All Stars XI huko Thailand, Julai 17. Msaidizi wa zamani wa Mourinho, Andre Villas-Boas, alisema anaamini kocha huyo ameshasaini mkataba mpya. Kocha huyo wa Tottenham, ambaye aliwahi kufanya kazi kwenye klabu alizopitia Mourinho, Porto na Chelsea alisema: "Nina uhakika uamuzi wa mwisho umeshafanyika. Nadhani anafurahi kurudi England, ni kama nyumbani kwake. "Huwa si jambo la kawaida kuona mtu akisema ataondoka kwenye klabu fulani wakati hajakamilisha mipango." Villas-Boas aliongeza: "Ana historia nzuri kwenye ligi hii, nadhani atatoa changamoto baada ya kuwasili hapa. Wachezaji wanampenda na wamekuwa wakitaja jina lake mara kwa mara." Akiwa Chelsea, Mourinho alipata ubingwa wa Ligi Kuu England msimu wa 2004/2005 na 2005/2006 pia alipata Kombe la FA msimu wa 2006/2007. Alipata vikombe vya ligi msimu wa 2004/2005, 2006/2007 na Ngao ya Hisani, 2005. |