Wapo
watu ambao ni wa kwanza kuwaumiza wenzao lakini wao wakiumizwa ni
matatizo tupu! Wanajihisi kama wao pekee ndiyo wenye moyo wa kuumia
lakini wenzao hawapati maumivu. Hivi hii inaingia akilini kweli?
Marafiki
zangu, lazima tufahamu kwamba mioyo yote ina nyama. Kuna mambo mengi
ambayo mpenzi akifanyiwa na mwenzake lazima ataumia sana. Ingawa kuna
mengine yanafichwa au kupasishwa kama sahihi, lakini ukweli unabaki pale
pale kwamba yanaumiza.
Kikubwa
ambacho unatakiwa kufahamu ni kwamba maumivu hayo yapo sawa kwa kila
mmoja. Haijalishi jinsia, umri, kabila wala dini, maumivu ya mapenzi
yote yanafanana. Kufanana huko kunasababishwa na mioyo yote kuwa na
nyama!Kwa
sababu mioyo yote ina nyama basi unatakiwa kufahamu kwamba, jinsi
unavyoumia wewe moyoni mwako, ndivyo mpenzi wako anavyoumia ikiwa
utamfanyia makosa kama ambayo unamfanyia wewe.
UMEWAHI KUWAZA KUHUSU KUSALITIWA?
Unajua
kabisa una mpenzi, tena inawezekana wakati mwingine mmeshawahi
kuzungumza juu ya kuishi pamoja, lakini bila haya wala aibu, unamsaliti!
Kwa nini unafanya hivyo? Kama umeona hana thamani tena kwako, kwa nini
unazidi kumpotezea muda?
Unafikiri
anafurahia sana wewe kuwa na kimada mwingine huko uchochoroni au
unadhani atafurahia siku akijua kuwa una mtoto umezaa nje ya ndoa yako?
Nafsi yako yenyewe inakusuta, inajua ni kiasi gani unamkosea mpenzi wako
lakini unajifanya kichwa ngumu na kuendelea na uchafu wako. Kwa nini
hutaki kubadilika?
Hebu
jitoe katika nafasi yako, kisha mfanye mpenzi wako ndiyo wewe, halafu
fikiria kama yeye ndiyo angekuwa anakusaliti, ungejikiaje? Lazima
utaumia! Sasa kama utaumia kwa nini unaendelea kumfanya mwenzako akose
raha?
Lazima
uwe na moyo wa huruma, akili yako ifanye kazi ipasavyo na kugundua
makosa unayoyafanya kisha kufanya mabadiliko ya haraka. Amini jinsi
utakavyoumia kwa kufanyiwa mabaya na mwenzako ndivyo mpenzio anavyoumia
kwa mabaya unayoyafanya.
Wengi
wamekuwa wakiwasaliti wapenzi wao wakiwa hawafikirii siku ya wao
kufanyiwa hivyo itakavyokuwa. Hebu vuta picha, unakwenda nyumbani kwa
mpenzi wako, unagonga mlango haufunguliwi!
Baadaye
unahisi kama ndani kuna watu, hilo linaingia akilini mwako baada ya
kuona viatu vya mpenzi wako pamoja na viatu vingine vya jinsia tofauti
ya mpenzi wako.
Unaamua
kusukuma mlango na kuingia ndani, hamadi! Unakuta mpenzio akiwa
kitandani na mtu mwingine. Utajisikiaje? Jiweke katika nafasi hiyo.
Naamini kabisa ni lazima utajisikia vibaya sana, sasa kama ndivyo, kwa
nini wewe unamsaliti?
Mapenzi
ya kweli hayaambatani na usaliti. Penzi la kweli lina uaminifu wa
dhati, kuchukuliana, kupendana, kusaidiana, ukarimu, huruma na mengine
mengi ambayo huyafanya mapenzi yazidi kuwa imara kila siku.
USIJIFIKIRIE MWENYEWE...
Vipengele
vilivyopita vinafafanua hili kwa undani, lakini kwa kuongezea ni kwamba
huna sababu ya kujiwazia wewe mwenyewe! Kujiona wewe pekee ndiye mwenye
haki ya kuwa salama katika penzi lako.
Chunga
nafsi yako lakini wakati huo huo ukiangalia kwa jicho la tatu, nafsi ya
mwenzako. Kila mmoja anaumia anapohisi kusalitiwa, hivi unafikiri ni
nani anayependa kushea mapenzi? Hakuna.
Utakuta
mwingine simu ya mpenzi wake ikiita anakuwa wa kwanza kuichukua na
kutaka kupokea au kusoma sms, lakini subiri sasa simu yake iite; Anakuwa
mkali zaidi ya mbogo! Acha kujifikiria peke yako.
KIPO CHA KUFANYA!
Siamini
kama kuna ambacho sijaandika katika vipengele vyote vilivyopita, lakini
hapa nakusisitizia kufanya mabadiliko ya haraka ili mwisho wa siku
uweze kuishi maisha mapya, mazuri, yenye mapenzi ya kweli huku moyo wako
ukiwa huru.
Hutakuwa
na maumivu moyoni mwako, maana utakuwa unamtendea haki mpenzi wako.
Lakini kama ukiendelea kumsaliti, ujue wazi kwamba utakuwa unajizidishia
maumivu katika moyo wako.
Huo ndiyo ukweli!