Headlines News :

Tuesday, September 24, 2013

CHOMBEZO : FACEBOOK CHATTIN' - 2



MWANDISHI: NYEMO CHILONGANI
0718 069 269.

Mtu mzima nikaingia kazini kwa ajili ya kuanza kazi yangu ambayo nilikuwa nimepewa ya kuhakikisha kwamba mtoto wa Kipemba, Aziza anakuwa wangu. Ni kweli kwa mambo ambayo alikuwa amenieleza Eduado yalikuwa yamekwishanitenga kwa kiasi kikubwa sana kutoka kwa Aziza lakini ilitakiwa pia nifanye yangu katika kipindi hicho.
Kitendo cha Aziza kuikubali Friend request yangu kilionekana kuwa kitu kizuri sana, kwa hiyo nilichokifanya nikajifanya bonge la bwege, nikamfuata kwa wall yake na kuandika ‘thanx A’ na kisha kusikilizia.
Kweli, kama alivyosema Eduado ilikuwa vile vile, demu hakuiLIKE thanx yangu wala kuitolea comment, nikaona poa, vyote hivi ni mwanzo wa kumbukumbu zangu nitakazompa hapo baadae. Kwa upande wa Eduado, hakutaka kujishika, kila siku alikuwa akinisumbua tu kwa inbox.
EDUADO: Kaka vipi?
MIMI: Kuhusu nini?
EDUADO: Mtoto. Hujaniambia chochote kile. Umefanikiwa au?
MIMI: Wewe umeniambia mambo mengi kuhusiana na huyu mrembo, unadhani ningeweza kumamilisha ndani ya siku tatu?
EDUADO: Hapana. Nilikuwa nauliza manake nimeona hapa sasa hivi u rafiki yake.
MIMI: Yeah! Ni rafiki yangu ila kila kitu kinatakiwa kufanywa kimahesabu.
EDUADO: Usianiangushe basi Sharukh Khan.
MIMI: Hilo usijali.

Katika kipindi hicho nilikuwa nafikiria mambo mengi sana, huyu mtoto kwangu alionekana kuwa na pozi ajabu, yaani nilikuwa nikizipitia post za kizushi alizokuwa akiziweka, watu walikuwa wakicomment halafu yeye hatokei. Hata kama kaweka picha ya mdoli, watu walikuwa wakicomment halafu yeye hatokei na mbaya zaidi kulikuwa na watu wengi wanaolike na kucomment jambo lililonifanya kugundua kwamba kuna siku huyu msichana alikwishawahi kuweka picha na hivyo wanaume kujua ni mzuri na kisha kuzitoa.
Bado kiu yangu ilikuwa ni kuwasiliana na Aziza tu ambaye alionekana kuwa mtu wa mapozi sana. Sikujua ningeanzia wapi ila nilichokifanya ni kuanza kumtumia meseji nione kama angeijibu au kuipotezea.

MIMI: Mambo!
Niliituma meseji hiyo, siku ya kwanza, ya pili, ya tatu mpaka wiki hadi mwezi lakini meseji ile moja haikujibiwa, mbaya zaidi nilikuwa namuona online. Sikukoma kidume mimi, bado nilikuwa nikimtumia meseji za kumsalimia lakini hali ilikuwa vile vile, hakujibu.
Mtu mzima nikaona naumbuka, kama nilikuwa naitwa Sharukh Khan basi ilibidi niwaonyeshe watu kwamba hawakukosea kuniita jina hilo, nilitaka kuwaonyeshea dhahiri kwamba mama yangu alikuwa mtu wa Tanga, kule ambapo mapenzi yalikuwa yamenogeshwa kwa kuwekewa makorokocho. Nilichoanza kukifanya ni kuanza kumtag picha. Hapa ni lazima ugundue, picha ambazo nilikuwa nikimtag ni zile ambazo zilikuwa romantic tu. Picha ambazo zilikuwa zikiwaonyesha wapenzi wakibusiana na kukumbatiana, ndizo ambazo nilikuwa nikimtag, tena yeye peke yake.
Hahaha! Ule ukaonekana kama ujinga vile kumbe kwa wakati huo nilikuwa na target zangu kichwani. Niliendelea na mtindo ule ule mpaka siku ambayo akaonekana kuchoka na kukasirika, kwa mara ya kwanza akaja inbox, ila sio kiamani kama nilivyotaka, alikuja kibifu.

AZIZA: Naomba usiwe unanitag mapicha yako.

Niliisoma meseji ile. Kwanza nikacheka, kilichonifanya kucheka ni kwa kumuona kwamba alikuwa msichana mjinga sana, kitendo cha yeye kuniandikia meseji kilionekana kuwa kama kosa kubwa sana, nilichokifanya, nikaanza kuandika meseji ndefu, meseji ambayo ingemfanya kunijibu, meseji ambayo isingemfanya kubaki kimya.
MIMI: Kuna vitu kadhaa Aziza itakupasa uelewe na ninatumaini vitakuongoza katika maisha yako yote. Jitahidi kuishi lakini kamwe usiwe mbinafsi. Unapopata kitu, usitake kukaa nacho, jaribu kuchangia pamoja na wenzako. Unapopata chakula, jaribu kumwangalia yule asiye na chakula na kumgawia, milele atakushukuru kwa ulichomfanyia. Unapomuona mtu hana nguo, mgawie nguo na ataendelea kukushukuru maisha yake yote. Unaniona mimi, mimi si mbinafsi hata mara moja, katika maisha yangu nimekuwa nikiwapa watu vitu fulani vitu ambavyo hawana katika maisha yao, nikakuangalia wewe, nikakuona kwamba u masikini sana, ukijiangalia, unajiona kuwa tajiri, mwenye fedha labda, lakini bado ni masikini, masikini wa kitu kimoja ambacho ulihitaji mtu mwenye kitu hicho akusaidie, nikakusaidia lakini unaonekana kuukataa msaada wangu. Kuwa makini Aziza, mara nyingine msaada huja mara moja na kupotea, unapoutafuta, inawezekana usiuone tena.

Kwanza nikashusha pumzi nzito, nikaiangalia meseji ile na kisha kuirudia rudia mara nyingi nyingi na kisha kuituma. Niliiona kuwa meseji kali ambayo isingemfanya kubaki kimya kwa kutaka kujua ni kitu gani ambacho alikuwa amekosa katika maisha yake, kilichonifurahisha, akatuma meseji. Kuna nini tena? Meseji ya pili hiyo, hakujua kwamba ndio mwanzo wa chating yetu.
AZIZA: Umemaanisha nini?
MIMI: Nimemaanisha kwamba wewe ni masikini. Tena yule fukara kabisa. Hiyo ndio maana yangu.
AZIZA: Sijakuelewa.
MIMI: Hebu isome vizuri hiyo meseji, utaielewa tu.
AZIZA: Nimeirudia zaidi ya mara tano, sijaielewa, naomba uniambie umemaanisha nini.
MIMI: Nikuulize kitu kimoja?
AZIZA: Niulize.
MIMI: Unaweza kugundua ni umasikini wa aina gani umekuwa nao?
AZIZA: Hapana na ndio maana nikauliza.
MIMI: Inawezekana mkawa na magari, nyumba na fedha ila bado ukawa masikini, unakubaliana nami?
AZIZA: Hapana.
MIMI: Kwa sababu gani?
AZIZA: Mtu ana kila kitu, atakuwaje masikini.
MIMI: Hahahah! Aziza. Ukisema hivyo unakosea. Kuwa na kila kitu haimaanishi kwamba wewe si masikini. Unaniruhusu nikuulize kitu?
AZIZA: Niulize
MIMI: Unaamini katika fedha?
AZIZA: Yeah!
MIMI: Fedha inaweza kukupa kila ukitakacho?
AZIZA: Yeah!
MIMI: Unakosea sana Aziza.
AZIZA: Unapokuwa na fedha unanunua gari ulitakalo, unanunua chakula, unanunua nyumba na mambo mengine. Kwani nimekosea?
MIMI: Umepatia. Ila unavyoona kila mtu mwenye fedha huwa na furaha?
AZIZA: Inawezekana.
MIMI: Umekosea. Umekwishawahi kuwasikia wale matajiri wanaojiua?
AZIZA: Yeah!
MMI: Sasa wamekosa nini wale katika maisha yao? Wana fedha, wanaweza kununua kila kitu, wana magari, wanaweza kwenda sehemu yoyote ile. Ila swali linakuja kwa sababu gani walijiua?
AZIZA: Mmmh! Sijui.
MIMI: Hahaha! Jibu rahisi sana. Walikosa furaha, amani, wakakosa mapenzi na mambo mengine. Unapokuwa na fedha, utanunua gari ila kumbuka hautoweza kununua furaha, unapokuwa na fedha utaweza kumnunua msichana mtaani lakini ukashindwa kununua mapenzi. Umenipata hapo?
AZIZA: Kidogoooo.
MIMI: Yeah! Kila mtu hunipata kidogo, ila tukiendelea kuchati, utanipata sana tu. Utaniruhusu niwe nachati nawe kwa ajili ya kukuambia mengi usiyoyajua?
AZIZA: Yeah! Ila huwa siwi online muda wote.
MIMI: Hilo si tatizo. Unachotakiwa ni kunishtua kila unapokuwa online. Utakwenda kufahamu mengi ambayo haujayajua. Kwani unaishi wapi?
AZIZA: Nipo Masaki Dar es Salaam.
MIMI: Ndio maana.
AZIZA: Kwa nini?
MIMI: Usijali. Mtaa unaokaa ndio nitakaoanza nao siku tukianza kuchati. Kwa sasa nahitaji kusoma, naomba uniruhusu niondoke.
AZIZA: Ila pleeeaseeee naomba uniambie.
MIMI: Sijakataa. Nitakwambia tu wala usijali. Wewe ni rafiki yangu, pamoja kuwa na kila kitu, yakupasa kupata vitu vingine ambavyo haupaswi kuvinunua. Nitakwambia namna ya kuvipata na inawezekana hata marafiki zako wakakushangaa.
AZIZA: Mmmh!
MIMI: Usigune. Huo ndio ukweli. Usiku mwema Aziza.
AZIZA: Nawe pia.

Kuna nini tena? Nilichokifanya ni kutoka online mpaka saa sita ndio nikaingia tena, Aziza hakuwepo, nikamtafuta Eduado, nikamuona, hata kabla sijamtumia meseji, akaniwahi.
EDUADO: Vipi Sharukh Khan. Imekuwaje au bado?
MIMI: Kwisha habari yake. Anacheza na mwanasaikolojia nini.
EDUADO: Imekuwaje tena?
MIMI: Wewe usijali. Cha msingi andaa zawadi yangu.
EDUADO: Umeanza kufanikisha?
MIMI: Ndio maana yake. Unajua ukimjua mpinzani inakuwa rahisi sana.
EDUADO: Dah! Wewe noma kaka. Yaani hii kazi nimewapa watu saba, naona wengine wanambwela tu, wananiambia kila wakimtumia meseji dogo hajibu.
MIMI: Hahahaha! Hata mimi ilikuwa hivyo hivyo. Nilivyoona anashindwa kujibu, nikatumia plan B. Hapo ndipo nilipompoteza na kuchati nae sana.
EDUADO: Kwa hiyo ulichati nae?
MIMI: Yeah! Tena mimi ndiye nimemkatisha. Chezea mimi wewe.
EDUADO: Hahahah! Ebwana wewe nomaaaaa....sasa hata kukutambulisha kwa demu wangu mwingine naogopa.
MIMI: Wewe si ulinipa kazi kaka? Hakuna tatizo. Kazi inafanyika taratibu.
EDUADO: Duh! Kaka nashukuru sana kwa kunisikiliza. Natumaini mtoto ataeleweka tu.
MIMI: Amekwishaeleweka. Dogo amekwishaeleweka.
EDUADO: Hahahah! Basi poa sana, nimefurahi sana.
MIMI: Usijali kaka...hug.
EDUADO: Poa.

Kila kitu kikaonekana kuwa juu ya mstari, meseji moja ambayo alikuwa amenitumia ikaonekana kubadilisha kila kitu. Ile meseji ndio ambayo nilikuwa nikiitaka kuiona na kweli aliituma. Chattin zikawa zimeanza, kwa Aziza, nilihitajika kuwa makini sana kupita kawaida kwani kwa kufanya vile nilikuwa na uhakika wa kumchukua ili kumuonyeshea Eduado kwamba nilikuwa Sharukh Khan.


Je nini kitaendelea?
  •  
    Support : Blog designer | Blogger | Developer | | KakyteeMedia.InC
    Copyright © 2011. Kakytee.com - All Rights Reserved
    Template Modified by KakyteeMedia
    Proudly powered by Blogger