Headlines News :

Sunday, April 28, 2013

JINSI YA KUMKABILI MWANAUME ASIYE CHAGUO LAKO!

Ni kweli kwamba, kila binadamu ana haki ya kupenda, hili halipingiki hata kidogo, lakini kulingana na mila na desturi zetu za Kiafrika wanaume ndio huwa waanzilishi wa uhusiano.
Kwa utamaduni huo basi, mwanamke hukosa uhuru wa kufikisha hisia zake kwa yule aliye chaguo lake huku mwanaume akiwa huru kutoa dukuduku lake pale anapohisi kupenda.
Pamoja na kwamba maendeleo ya sayansi na teknolojia yanamfanya mwanamke wa sasa awe na haki sawa na mwanaume, bado kumekuwa na ugumu kwa mwanamke kumwambia mwanaume kuwa anampenda na angependa kuwa mpenzi wake.
Mwanamke wa aina hiyo, huonekana mhuni, asiyejiheshimu. Lakini kuna jambo moja la msingi hapa kulijadili; ni pale mwanamke anapotongozwa na mwanaume asiye chaguo lake. Wakati mwingine inawezekana hata hajatongozwa, lakini dalili za mwanaume huyo zikamfanya aone wazi kwamba anamtaka ila yeye moyoni mwake akawa hana nafasi kabisa.
Hapa ndipo wanawake wengi wanapobaki njia panda. Kwa bahati mbaya sana, wapo ambao huamua kuingia kwenye uhusiano kwa majaribio, jambo ambalo ni hatari kwenye uhusiano.
Inapotokea hali hiyo baadhi ya wanawake wanashidwa kujua la kufanya na kufikiri labda kuwajibu majibu ya hovyo huweza kufikisha hisia zao na kuachwa kusumbuliwa.
Kama yupo mwanaume anayekusumbua mara kadhaa na wakati mwingine kuona kuwa ni kero kwako na hujui cha kufanya, usijali fungua ubongo ili uweze kuongeza kitu kipya. Kuna baadhi ya wanawake wanafikia hatua ya kuwatukana au kuwakejeli wanaume ambao wamekuwa wakiwasumbua kila wakati.
Usijali, kipo kitu cha kufanya. Zipo njia za kumweleza mwanaume husika humhitaji kistaarabu na yeye asijisikie vibaya na ukamuacha akiwa mwenye kukuheshimu siku zote za maisha yake.

NI MWANAMKE YUPI?

Kwanza lazima nifafanue aina ya mwanamke ninayemzungumzia hapa. Kama upo kwenye ndoa yako, vipengele vifuatavyo hapa chini havitakuhusu kabisa, maana mwanaume anayemtongoza mke wa mtu, jibu lake ni mhuni.
Hana staha na hafai kuthaminiwa na kupewa heshima ninayoizugumzia katika mada hii. Kwanza, mke wa mtu ana alama. Zipo nyingi na zinajulikana hasa kwa watu wanaomzunguka – wanamfahamu vizuri.
Ijulikane kwamba hata huyo mwanaume anayekutongoza, anakufahamu vizuri; ikiwa ni vinginevyo, huna sababu ya kujisumbua, huyo naye ni mhuni tu. Unajua kuna baadhi ya wanaume, hawapitwi.
Kila mwanamke anayemuona mbele yake, anamtaka. Hao siyo ninaowazungumzia katika mada hii. Rafiki yangu, kama upo kwenye uchumba, una mwenzako anayejulikana au hata kama hajulikani, jibu lako ni jepesi tu, una mchumba!
Hutakuwa na sababu ya kutumia njia hii. Njia hii ni kwa wanawake ambao wako huru – wanasaka waume wa maisha yao, lakini kwa bahati mbaya, mwanaume aliyekutamkia mapenzi, si cha chaguo lake.
Nimetoa angalizo hilo kwa sababu, wanawake ambao tayari wako kwenye miliki za watu, si busara kuruhusu mawasiliano au mikutano na watu wasio wao, tena kuzungumzia mapenzi. Naamini nimeeleweka vyema. Sasa tuendelee...

MSIKILIZE
Hili linawashinda wengi, lakini waswahili walisema kubali wito, kataa neno. Kumsikiliza hakuna maana kuwa tayari umeshamkubalia. Kutana naye lakini jitahidi kukwepa sehemu zenye vificho au ambazo utakuwa na wasiwasi nazo. Kukubali kwako kutamfanya mwanaume huyu aone kuwa hujamdharau na unamheshimu.



MPE UHURU AJIELEZE
Mwingine anaweza kufaulu vizuri hatua ya kwanza ya kukubali wito, ila akifika tu ataanza: “Sema haraka ulikuwa unasemaje?” au “Nina haraka bwana zungumza haraka ulichoniitia,” na maneno mengine mengi yanayofanana na hayo.
Hayo siyo mambo, mwache azungumze, onyesha kujali mazungumzo yake na kuwa makini kwa kila anachozungumza japokuwa tayari moyoni unatambua kuwa haupo tayari kuwa naye.
Hakikisha anafahamu kuwa mawazo yako yapo pale, hii itamfanya jamaa kuwa huru kwako na kukueleza hisia zake kwa uwazi zaidi – si ajabu ukabadilisha mawazo! Wiki ijayo tutaendelea na mada hii, USIKOSE!

  •  
    Support : Blog designer | Blogger | Developer | | KakyteeMedia.InC
    Copyright © 2011. Kakytee.com - All Rights Reserved
    Template Modified by KakyteeMedia
    Proudly powered by Blogger